Makamu wa Rais Tanzania: Kuharibu mazingira ni kumkufuru Mungu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Bi Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuacha kumkufuru Mwenyezi Mungu katika uumbaji wake kwa kuharibu mazingira ili kwa njia hiyo kuendelea kulinda ikolojia.
Bi Samia ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe baada ya kuzindua shamba la miti la Iyondo-Mswima katika eneo la Katengele, ambapo amesema kuwa kuharibu mazingira ni kumkufuru Mungu. “Kuharibu alichokileta Mwenyezi Mungu kiwafae wanadamu huku mkiwa mnaenda misikitini na makanisani ni kumkufuru Yeye.” Amesema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania. Ameeleza kusikitishwa na shughuli za kibinadamu katika baadhi ya maeneo aliyoyapitia ndani ya wilaya ya Ileje ambapo kilimo kinaendeshwa kando ya mito bila kujali sheria zinazolinda mito.
Ameongeza kwa kusema kuwa, iwapo sheria hizo hazitazingatiwa basi iko hatari ya milima mingi kubaki vipara kwani kinachofanyika si ukataji miti kwa malengo ya kutunza akiba bali ni unyoaji wa miti hiyo. Ameenda mbali na kusisitiza kwamba, kamwe kilimo kisiwe kisingizio cha kuharibu mazingira kwa kuwa uharibifu wa mtu mmoja huleta madhara kwa watu wengi.