Misri yatoa hukumu ya kunyongwa wafuasi 75 wa Ikhwanul Muslimin
Mahakama ya Misri leo imetoa hukumu ya kunyongwa wafuasi 75 wa chama cha Ikhwanul Muslimin na sasa hukumu hiyo inasubiri idhini ya mufti wa nchi hiyo kabla ya kutekelezwa.
Taarifa zinasema, mahakama hiyo ambayo ilikuwa na kikao chake mjini Cairo chini ya uwenyekiti wa Jaji Hassan Farid imetoa hukumu baada ya kusikiliza kesi ya wafuasi wa Mohammad Mursi, rais wa zamani wa Misri aliyeondolewa madakrani na ambaye ni kati ya vinara wa Ikhwanul Muslimin. Kesi hiyo ilihusu mijumuiko wa mwaka 2013 katika medani ya Rabaa Adawiya mjini Cairo. Mjumuiko huo ulifanyika baada ya jeshi, chini ya uongozi wa Rais wa sasa wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, kumtimua Mursi kupitia njia yya mapinduzi. Katika makabiliano yaliyojiri katika medani hiyo kulalamikia kitendo cha kupinduliwa Mursi, mamia ya watu waliuawa wakati jeshi likitawanya waandamanaji.
Kati ya waliohukumiwa kifo na mahakama hiyo ni viongozi waandamizi wa Ikhwanul Muslimin, Mohammad Al Beltagui, Essam Al Erian, Abdul Rahman Al Bar na Osama Yassin.
Baada ya Mursi kupinduliwa, chama chake cha Ikhwanul Muslimin kilitangazwa kuwa kundi la kigaidi na wafuasi wake wengi, akiwemo Mursi mwenyewe wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka katika mahakama za nchi hiyo huku wengi wakihukumiwa kunyongwa.
Baada ya kupinduliwa Mursi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri, nafasi yake ilichukuliwa na El Sisi ambaye anawakandamiza wapinzani kwa kutumia mkono wa chuma, jambo ambalo limepelekea ghasia na machafuko kuenea katika nchi hiyo.