Serikali ya Tanzania yaamuru msako wa kuwakamata wahamiaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47285-serikali_ya_tanzania_yaamuru_msako_wa_kuwakamata_wahamiaji
Serikali ya Tanzania kupitia mkuu wa mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga imeitaka idara ya uhamiaji kuanza msako mkali kwa ajili ya kuwakamata wahamiaji haramu waliojificha katika mashamba na majumbani mwa watu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 07, 2018 03:17 UTC
  • Serikali ya Tanzania yaamuru msako wa kuwakamata wahamiaji

Serikali ya Tanzania kupitia mkuu wa mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga imeitaka idara ya uhamiaji kuanza msako mkali kwa ajili ya kuwakamata wahamiaji haramu waliojificha katika mashamba na majumbani mwa watu.

Maganga ametoa agizo hilo kwenye sherehe za kuwaapisha wakuu wa wilaya ya Kasulu na Buhigwe zilizofanyika jana Jumatatu. Akifafanua suala hilo mkuu wa mkoa wa Kigoma amesema kuwa, wahamiaji haramu mkoani humo wanatakiwa kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili wahukumiwe kifungo na watumikishwe. "Watakaobainika kuvunja sheria wafungwe na huko wakafanye kazi hasa katika kipindi hiki cha kufufua mashamba ya michikichi, sio wakakae tu magerezani, na wakimaliza kifungo warudishwe katika nchi zao", amesema. Kadhalika Emmanuel Maganga ameiomba mahakama kuhakikisha kesi zote za wahamiaji haramu zinapewa kipaumbele ili kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani, ambao wanakula chakula bila kuzalisha.

Wakimbizi wa Burundi

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa serikali, kuna wahamiaji haramu na wakimbizi waliotoroka kambini na wanaishi mitaani na kwenye nyumba za watu kinyume cha sheria, jambo ambalo halikubaliki. Katika sehemu nyingine amesema kuwa, amesema kuwa si kila mtu mwenye hati ya kusafiria au kitambulisho cha kupiga kura atapata kitambulisho cha Taifa.

Msako huo dhidi ya wahamiaji umetangazwa katika hali ambayo kwa mara kadhaa viongozi wa upinzani akiwemo Zitto Zuberi Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini, kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo, amekuwa akilalamikia mwenendo huo wa msako ambao umekuwa unawalenga raia pekee wa mkoa huo kinyume na raia wa mikoa mingine inayopakana nan chi jirani.