Aug 12, 2018 14:54 UTC
  • Waasi wa Ethiopia watangaza kusimamisha mapigano kufuatia mageuzi ya serikali

Kundi moja la waasi nchini Ethiopia leo Jumapili limetangaza usitishaji mapigano wa upande mmoja, hatua iliyotajwa na weledi wa mambo kuwa ina lengo la kuhitimisha uhasama kufuatia mageuzi yanayofanywa na serikali ya Addis Ababa.

Waasi wa Harakati ya Taifa ya Ukombozi wa Ogaden (ONLF) mwaka 1984 walianzisha mapigano ya kujitenga mkoa wa Somalia unaojulikana pia kwa jina la "Ogaden" huko mashariki mwa Ethiopia. Mwaka 2007 vikosi vya jeshi la Ethiopia vilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya waasi hao baada ya kundi hilo kukishambulia kituo kimoja cha mafuta cha Wachina na kuuwa watu 74.

Ifahamike kuwa, harakati ya waasi hao wa Ethiopia wa ONLF ni miongoni mwa makundi mawili yaliyoondolewa na Bunge la Ethiopia katika orodha ya harakati zilizopigwa marufuku. Hatua hiyo imechukuliwa katika sehemu ya mageuzi yanayoongozwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ambaye amewanyooshea wapinzani mkono wa kutaka suluhu na amani.

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia 

Katika taarifa yao, waasi wa Ogaden wamesema kuwa wamezingatia hatua nzuri zilizochukuliwa na serikali ya Ethiopia za kuandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo na mapatano ya amani. Wameongeza kuwa watasimamisha oparesheni zote za kijeshi ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mzozo wa eneo la Ogaden.

Tags