Kiongozi wa Ikhwanul Muslimina ahukumiwa kifungo cha maisha jela, Misri
(last modified Mon, 13 Aug 2018 02:52:54 GMT )
Aug 13, 2018 02:52 UTC
  • Kiongozi wa Ikhwanul Muslimina ahukumiwa kifungo cha maisha jela, Misri

Kiongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimina ya Misri na maafisa wengine kadhaa wa ngazi za juu wa harakati hiyo wamehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa tuhuma za kuchochea mauaji na machafuko katika ghasia zilizotokea nchini humo miaka mitano iliyopita.

Mahakama ya Makosa ya Jinai ya Giza imemhukumu kifungo cha maisha jela Mohammed Badie na viongozi wengine kadhaa wa ngazi za juu wa harakati ya Ikhwanul Muslimin akiwemo Mohamed el-Beltagy, Safwat Hegazy, Essam el-Erian na al-Husseini Antar kwa madai kwamba walichochea machafuko yaliyotokea katika mtaa za al Bahrul A'dham katika mji wa Giza ulioko kandokando ya jiji la Cairo. 

Mahakama hiyo pia imemhukumu kifungo cha miaka 15 jela Bassem Odeh na kifungo cha miaka 10 jela Ahmed Zahi, Hisham kamel na Jamal Fathi ambao wote ni wanachama wa harakati ya Ikhwanul Muslimin. 

Majaji wa mahakama hiyo wamedai kwamba, viongozi hao wa harakati kubwa zaidi ya kisiasa ya upinzani iliyopigwa marufuku nchini Misri wamepatikana na hatia ya kuchochea mauaji, kufanya vitendo vya kigaidi na kuharibu mali ya umma na ya watu binafsi baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani aliyekuwa rais halali wa nchi hiyo, Muhammad Mursi. 

Mursi anashikiliwa katika jela ya utawala wa Misri

Harakati ya Ikhwanul Muslimin ilipigwa marufuku na kuwekwa katika orodha ya makundi ya kigaidi baada ya mapinduzi ya jeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Mursi Julai mwaka 2013. 

Tags