UN yatahadharisha kuhusu kufukuzwa wakimbizi huko Libya
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetahadharisha kuhusu kufukuzwa wakimbizi 1,900 huko Libya.
UNHCR leo Jumatano imetangaza kuwa wanamgambo wamewafukuza wakimbizi 1,900 katika kambi iliyoko katika eneo la Tariq al Mattar huko Tripoli mji mkuu wa Libya.
Taarifa ya shirika hilo imetoa wito wa kuheshimiwa haki za binadamu, kulindwa raia na kuheshimiwa haki za wakimbizi kwa ajili ya kuchukua maamuzi kuhusu mustakbali wao.
Kambi hiyo ya wakimbizi inayopatikana katika eneo la Tariq al Mattar iliasisiwa mwaka 2011 na kitendo cha kufukuzwa wakimbizi 1900 katika kambi hiyo kina maana ya kuivunja kikamilifu kambi hiyo.
Familia karibu 370 zinaishi kwenye kambi hiyo. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, wakimbizi 704 kutoka nchi 40 wanaishi Libya. Wahajiri haramu hutumia njia ya Libya kama nukta kuu ya kuingia Ulaya kupitia bahari ya Mediterania.
Idadi ya wahajiri haramu imeongezeka pakubwa katika kambi mbalimbali zinazowahifadhi raia hao wa kigeni huko Libya. Aidha maelfu ya wahajiri hao ambao wameokolewa baharini au kutiwa mbaroni na vyombo vya usalama vya Libya wamesajiliwa nchini humo.