Kipindupindu chaua watu 22 nchini Niger
Wizara ya Afya ya Niger imesema kuwa, watu wasiopungua 22 wamepoteza maisha kutokana na mripuko mpya wa kipindupindu nchini humo.
Wizara hiyo imetangaza kuwa, wimbi jipya la ugonjwa huo limeliathiri zaidi eneo la Maradi la kusini mwa Niger tangu mwezi Julai mwaka huu na hadi hivi sasa watu 22 wameshapoteza maisha kutokana na ugonjwa huo wa kuambukiza.
Wizara ya Afya ya Niger aidha imesema, waliothiriwa zaidi na ugonjwa huo ni wanawake na watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea.
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 54 ya wanawake ndio waliokumbwa na kipindupindu huko Niger na kesi 372 za ugonjwa huo zimewakumba watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea.
Takwimu rasmi zinaonesha kwamba, kiwango cha vifo vinavyotokana na kipindupindu ni asilimia 4.5 nchini Niger.
Kipindupindu ni ugonjwa hatari unaosababishwa na bakteria hasa katika utumbo mwembamba. Bakteria hao ambao huitwa vibriocholerae huweza kusababisha kuhara sana na kutapika kupindukia pamoja na homa kali.
Maambukizi ya kipindupindu hutokea hasa kupitia maji au vyakula vilivyochafuliwa na wadudu kama vile nzi.
Wadudu hao huweza kuchafua vyakula endapo vyakula hivyo vitaachwa wazi bila kufunikwa na chombo chochote na kuvutia nzi hao kutua juu ya vyakula hivyo na kuacha bakteria watakaosababisha ugonjwa wa kipindupindu kwa mtu atakayekula chakula hicho.