Makumi ya watu wahukumiwa kifo kwa kuua wapinzani wa Gaddafi nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47475-makumi_ya_watu_wahukumiwa_kifo_kwa_kuua_wapinzani_wa_gaddafi_nchini_libya
Mahakama moja nchini Libya imewahukumu adhabu ya kifo makumi ya watu baada ya kuwapata na hatia ya kuua waandamanaji waliokuwa wanapinga utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Aug 16, 2018 03:06 UTC
  • Makumi ya watu wahukumiwa kifo kwa kuua wapinzani wa Gaddafi nchini Libya

Mahakama moja nchini Libya imewahukumu adhabu ya kifo makumi ya watu baada ya kuwapata na hatia ya kuua waandamanaji waliokuwa wanapinga utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Shirika la habari la AFP limeinukuu Wizara ya Mahakama ya Libya ikisema kuwa, mahakama ya nchi hiyo imewahukumu adhabu ya kifo watu 45 baada ya kuwapata na hatia ya kuua waandamanaji waliokuwa wanapinga utawala wa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011 mjini Tripoli.

Wakati huo huo kitendo cha genge moja lenye silaha cha kumteka nyara mkazi wa eneo moja mjini Tripoli Libya, kimewakasirisha mno wakazi wa eneo hilo na kuamua kufunga barabara kuu ya kuingia mjini humo kwa siku ya pili mfululizo.

Mtandao wa al Bawabat al Afriqiyyah umezinukuu duru za usalama za Libya zikisema jana kuwa, watu hao wenye hasira wamewekwa vizuizi katika barabara kuu ya al Shatt al Trablus wakishinikiza kukomeshwa mara moja vitendo vya utekaji nyara mjini humo.

Miji ya Libya imeharibiwa vibaya sana baada ya uvamizi wa kijeshi wa NATO na Marekani

 

Libya ilitumbukia kwenye machafuko mwaka 2011 baada ya Marekani na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo katika kampeni za kuungasha utawala wa Kanali Muammar Gaddafi. Katika uvamizi huo, NATO na Marekani zilishambulia kinyama miundombinu ya Libya na kuivuruga kabisa.

Baada ya hapo ziliitelekeza nchi hiyo ya Kiarabu ya Kaskazini mwa Afrika baada ya kulivunja jeshi lake, na kuacha silaha zikiwa zimetapakaa mikononi mwa makundi hasimu ambayo kila moja lilikuwa linataka kuwa na nafasi kubwa zaidi nchini humo. Hivyo tangu wakati huo hadi hivi sasa nchi hiyo imeshindwa kuwa na utulivu wa angalau siku moja. Mivutano baina ya makundi mbalimbali yanayoungwa mkono na madola ajinabi ni sababu kuu ya kukosekana utulivu huko Libya.