Aug 18, 2018 07:34 UTC
  • Watoto 33 wafariki katika kambi za wakimbizi wa ndani nchini Nigeria

Watoto wasiopungua 33 wamepoteza maisha katika kipindi cha wiki mbili kati ya tarehe 2 na 15 Agosti katika kambi moja ya wakimbizi wa ndani ya nchi (IDP) kaskazini mwa Nigeria.

Hiyo ni kambi ya wakimbizi waliofukuzwa makwao kufuatia kuzuka kwa ugaidi wa kundi la magaidi wakufurishaji wa Boko Haram.

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, limesema kuwa limeweka mpango wa misaada ya dharura kwa wakimbizi wa kambi hiyo, iliyoko Bama, zamani mji wa pili wa jimbo la Borno. Tangu mwezi Aprili 2018, zaidi ya watu 10,000 wamewasili Bama, MSF imesema.

Pamoja na serikali ya Nigeria kudai kuwa hali imeanza kuboreka kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, kumeshuhudiwa ongezeko la mashambulizi na kusababisha kuzorota usalama katika eneo hilo.

Magaidi wa Boko Haram

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa, ambayo inatumiwa na aghalabu ya Waislamu wa Nigeria, lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

Tags