Raia 130 wauawa kwenye mapigano nchini Libya tangu mwaka 2018
Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa mambo ya kibinadamu nchini Libya Bi. Maria Ribiero, amesema raia130 wameuawa kwenye mapambano nchini Libya tangu mwaka 2018.
Kwenye taarifa, Bi .Ribiero amesema, tangu mwaka 2018, mapambano nchini Libya yamesababisha vifo vya raia 130 na wengine wengi kujeruhiwa, wakiwemo watoto.
Habari nyingine zinasema wizara ya sheria ya Libya imepinga malalamiko kutoka wapinzani wa kigeni kuhusu hukumu ya kifo iliyotolewa na mahakama kwa wafuasi 45 wa serikali ya Libya ya zamani.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo pia imezitaka pande mbalimbali husika, hasa mashirika ya kimataifa, zisiingilie mambo ya ndani ya Libya, hasa mambo ya kisheria. Mahakama ya Rufaa ya Libya siku ya Jumatatu ilitoa hukumu ya kifo kwa wafuasi 45 wa serikali ya zamani ya Muammar Gaddafi kutokana na mauaji ya waandamanaji mjini Tripoli mwaka 2011.

Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa na hali ya mchafukoge tangu kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi kufuatia uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO). Kwa sasa Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk na nyingine ni ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na ina makao yake mjini Tripoli.