Mbowe: Viongozi wa Chadema Tanzania, tunatengenezewa kesi ili tufungwe
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe, amesema kuwa, viongozi wa chama hicho wanatengenezewa kesi ili wafungwe jela na kusisitiza kuwa, pamoja na hayo wao hawaogopi kwenda jela.
Mbowe aliyasema hayo jioni ya jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu kesi inayowakabili yeye na baadhi ya viongozi wa chama chake. Alidai kuwa, viongozi wa Chadema kwa ujumla wameonyesha kutokuwa na imani na hakimu anayesimamia kesi yao, Wilbard Mashauri, kutokana na hakimu huyo kufanya kazi kwa maelekezo kutoka sehemu fulani yenye lengo la kutowatendea haki na kisha kuwafunga.
Mbowe alisema kama ninavyomnukuu: "Waliomuua Akwilina wapo, lakini tunatengenezewa kesi sisi ili tufungwe, tunasema hatuogopi kwenda jela, lakini tunataka tufungwe pale ambapo tuna haki ya kufungwa. Waue wengine, wapige risasi wengine, waumize wengine, walioonewa ndio wanakuwa washutumiwa?." Mwisho wa kunukuu. Amesema kwamba, kinachoendelea katika kesi hiyo wanayotuhumiwa kwa makosa 13 likiwemo la kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha msichana Akwilina, kiko wazi kwani hata ombi lao la kutaka kesi hiyo isikilizwe na Mahakama Kuu ya Tanzania, limetupiliwa mbali na kwamba hakimu ameamuru kesi hiyo ianze kusikilizwa na Mahakama ya Kisutu, jambo lililopelekea wakili wao wa upande wa utetezi, Jeremia Mtobesya, kujitoa.