Mbunge Bobi Wine ashindwa kufika mahakamani kwa sababu za kiafya
Mbunge Robert Kyagulanyi wa Kyadondo Mashariki nchini Uganda maarufu kama Bobi Wine, ameshindwa kuhudhuria mahakama hii leo kusikiliza kesi inayomkabili ya uhaini iliyowasilishwa na serikali ya nchi hiyo.
Wakili wa mwanasiasa huyo, Tonny Kitara amewambia waandishi wa habari kwamba mteja wake bado amelazwa katika hospitali moja ya mjini Kampala kufuatia majeraha aliyopata wakati alipokamatwa na askari wa serikali. Watuhumiwa wengine 25 ambao nao wameshitakiwa pamoja na Bobi Wine, walihudhuria mahakamani kusikiliza kesi yao. Katika faili hilo jumla ya watu 36 wameshtakiwa kwa makosa ya uhaini kufuatia madai kwamba, waliupiga kwa mawe msafara wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda.
Watuhumiwa wengine hawakuonekana mahakamani kwa kile ambacho mahakama ilielezwa kwamba, ni hali zao mbaya za kiafya na sababu nyingine. Habari zinasema kuwa, Bobi Wine atasafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu zaidi, ingawa bado haijajulikana ni nchi gani atapelekwa.
Bobi Wine pamoja na wabunge wengine wa upinzani alikamatwa na vyombo vya usalama vya serikali ya Uganda katikati ya mwezi huu unaomalizika, baada ya msafara wa magari wa Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni kushambuliwa kwa mawe. Askari wanaotuhumiwa kuwapiga na kuwatesa wabunge hao wa upinzani wametiwa mbaroni.