Idadi ya waliouawa katika mapigano ya Tripoli, Libya yafikia watu 41
Idadi ya watu waliopoteza maisha yao katika mapigano ya siku za hivi karibuni huko Tripoli, mji mkuu wa Libya imefikia watu 41.
Usiku wa kuamkia leo, hospitali ya Salahuddin ya mjini Tripoli imetangaza kuwa, watu 41 wameuawa na wengine 126 kujeruhiwa kutokana na mapigano makali yaliyozuka mjini humo hivi karibuni. Maafisa wa hospitali hiyo pia wamesema, kuna uwezekano wa kuongezeka idadi ya watu waliouawa kutokana na kuwa hali ya majeruhi 75 ni mahututi.
Wizara ya Afya ya Libya mapema jana Alkhamisi ilitangaza kuwa, watu 27 wameuawa na wengine 100 kujeruhiwa katika mapigano hayo. Mapigano mapya yalizuka mjini Tripoli Libya siku ya Jumapili baina ya makundi hasimu yenye silaha. Mapigano hayo yalisimama jana Alkhamisi baada ya kufikiwa makubaliano ya kusimamisha vita kati ya wakuu wa kikabila ingawa hadi hivi sasa hali bado ni ya wasiwasi na kuna uwezekano wa kuzuka tena mapigano.
Libya ilitumbukia kwenye machafuko mwaka 2011 baada ya Marekani na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo katika kampeni za kuungasha utawala wa Kanali Muammar Gaddafi. Katika uvamizi huo, NATO na Marekani zilishambulia kinyama miundombinu ya Libya na kuivuruga kabisa.
Baada ya hapo ziliitelekeza nchi hiyo ya Kiarabu ya Kaskazini mwa Afrika baada ya kulivunja jeshi lake, na kuacha silaha zikiwa zimetapakaa mikononi mwa makundi hasimu ambayo kila moja lilikuwa linataka kuwa na nafasi kubwa zaidi nchini humo. Hivyo tangu wakati huo hadi hivi sasa nchi hiyo imeshindwa kuwa na utulivu wa angalau siku moja. Mivutano baina ya makundi mbalimbali yanayoungwa mkono na madola ajinabi ni sababu kuu ya kukosekana utulivu huko Libya.