Mapigano yanaendelea Libya, uwanja wa ndege wa Tripoli wafungwa
Mapigano makali yanayoendelea mjini Tripoli yamepelekea kufungwa uwanja wa ndege wa mji mkuu huo wa Libya.
Vyombo vya habari vya kieneo vimewanukuu maafisa wa serikali wakitangaza jana usiku kuwa, wamelazimika kuufunga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mitiga wa mjini Tripoli kwa muda wa masaa 48 kutokana na kushadidi mapigano mjini humo na kwamba safari zote za ndege za uwanja huo zimehamishiwa katika uwanja mwingine wa ndege wa kimataifa wa Misrata.
Vyombo hivyo vya habari vimetangaza kuwa, risasi kadhaa zimepigwa ndani ya uwanja wa ndege wa Mitiga.
Tangu siku ya Jumapili hadi hivi sasa mji wa Tripoli umekuwa ni uwanja wa mapigano baina ya makundi hasimu. Licha ya mapigano hayo kusimama kwa muda siku ya Alkhamisi baada ya kufikiwa mapatano baina ya wakuu wa kikabila, lakini habari za kuendelea mapigano hayo zinaendelea kuripotiwa kiasi cha kufungwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji huo.
Alkhamisi usiku, hospitali ya Swalahuddin ya mjini Tripoli ilitangaza kuwa watu 41 wameuawa na 126 wengine wamejeruhiwa katika mapigano hayo.
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, mapigano hayo ya Tripoli yanaweza kusababisha machafuko katika kona zote za Libya.