Umoja wa Mataifa watoa wito wa kusitishwa haraka mapigano nchini Libya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kusitishwa haraka mapigano nchini Libya na pande zote zinazopigana katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ziheshimu usitishaji vita.
Antonio Guterres sambamba na kutoa wito huo amelaani vikali mapigano mapya yaliyopibuka katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli na kusisitiza kwamba, kuna haja ya pande husika kuheshimu makubaliano ya usitishaji mapigano.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba, pande zinazopigana nchini Libya zinapaswa kufungamana na makubaliano ya usitishaji vita yaliyofikiwa baina ya pande mbili chini ya usimamizi wa umoja huo.
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, mapigano hayo ya Tripoli yanaweza kusababisha machafuko katika kona zote za Libya.
Tangu siku ya Jumapili iliyopita hadi hivi sasa mji wa Tripoli umekuwa uwanja wa mapigano baina ya makundi hasimu. Licha ya mapigano hayo kusimama kwa muda siku ya Alkhamisi baada ya kufikiwa mapatano baina ya wakuu wa kikabila, lakini habari za kuendelea mapigano hayo zinaendelea kuripotiwa kiasi cha kufungwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji huo.
Alkhamisi usiku, hospitali ya Swalahuddin ya mjini Tripoli ilitangaza kuwa watu 41 wameuawa na 126 wengine wamejeruhiwa katika mapigano hayo.
Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa na hali ya mchafukoge tangu kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi kufuatia uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO).