Rais Sisi aidhinisha sheria inayodhibiti matumizi ya mitandao
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi ameidhinisha sheria mpya ya kudhibiti mitandao ya kijamii katika kile kinachotajwa kuwa ni muendelezo wa sera za kukandamiza upinzani.
Sheria hiyo mpya inaipa serikali haki ya kufuatilia watuamiaji wa mitandao ya kijamii nchini humo kama sehemu ya kuimarisha udhibiti wa mitandao.
Sheria hiyo imelipa nguvu kamili Baraza Kuu la Sheria za Vyombo vya Habari ambalo litakuwa na uwezo wa kuwaweka chini ya usimamizi watumiaji wa mitandao wenye wafuasi zaidi ya 5,000 - kwenye mitandao ya kijamii, blog binafsi au tovuti.
Aidha baraza hilo litakuwa na mamlaka ya kusimamisha au kuzuia akaunti yoyote binafsi ambayo "inachapisha au kutangaza habari bandia au taarifa yoyote inayochochea ukiukaji wa sheria, vurugu au chuki.
Itakumbukwa kuwa mwezi Juni 2013, Muhammad Mursi, rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia Misri kutoka harakati ya Ikhwanul Muslimin, aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali el-Sisi. Mursi aliingia madarakani kupitia uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Juni mwaka 2012 na baada ya kutimuliwa madarakani diktetea wa muda mrefu wa nchi hiyo Husni Mubarak mwaka 2011.
El-Sisi alishiriki katika uchaguzi uliofuata na kuchaguliwa ambapo baada ya hapo amewakandamiza wapinzani ikiwa ni pamoja na kuipiga marufuku Harakati ya Ikwanul Muslimin na kumfunga jela Mursi pamoja na idadi kubwa ya wafuasi wa harakati hiyo. Mwezi Machi el-Sisi alichaguliwa kwa muhula wa pili kwa asilimia 92 ya kura ambapo harakati ya Ikhwanul Muslimin ilipigwa marufuku na kuzuiwa kushiriki uchaguzi huo. El-Sisi amekuwa akitumia vyombo vya dola kukandamiza upinzani nchini humo.