Wafungwa zaidi ya 400 watoroka jela mjini Tripoli, Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47870-wafungwa_zaidi_ya_400_watoroka_jela_mjini_tripoli_libya
Wafungwa zaidi ya 400 wametoroka jela baada ya kuzuka uasi na machafuko katika jela moja iliyoko kwenye kiunga cha kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2018 03:24 UTC
  • Wafungwa zaidi ya 400 watoroka jela mjini Tripoli, Libya

Wafungwa zaidi ya 400 wametoroka jela baada ya kuzuka uasi na machafuko katika jela moja iliyoko kwenye kiunga cha kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Polisi ya Idara ya Mahakama ya Libya imetoa taarifa na kueleza kwamba, wafungwa hao walitoroka jana kwenye jela ya Ain Zara iliyoko kwenye kiunga cha kusini mwa Tripoli katika hali ambayo, tangu wiki moja iliyopita mji huo na kandokando yake umekuwa uwanja wa mapigano ya umwagaji damu kati ya makundi yanayobeba silaha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wafungwa walifungua milango ya jela hiyo kwa nguvu, hata hivyo ili kuepusha maafa na vifo, walinzi wa jela hawakuchua hatua yoyote ya kuwazuia wafungwa hao wasitoroke.

Kwa mujibu wa polisi ya Idara ya Mahakama ya Libya, wafuasi wa utawala uliopinduliwa wa Muammar Gaddafi, hasa wale waliofungwa kwa makosa ya mauaji yaliyofanywa wakati wa matukio yaliyopelekea kuangushwa utawala huo mwaka 2011 walikuwa wakishikiliwa kwenye jela hiyo ya Ain Zara.

Mapigano kati ya makundi yanayobeba silaha yamevuruga usalama mjini Tripoli

Kwa zaidi ya wiki moja sasa mji mkuu wa Libya Tripoli umekuwa uwanja wa mapigano kati ya makundi tofauti ya wanamgambo.

Siku ya Jumamosi, serikali ya mapatano ya kitaifa  ilitangaza kuwa usitishaji vita umeanza kutekelezwa, lakini hapo jana serikali hiyo ilitangaza hali ya hatari sambamba na kutoa indhari ya kuendelea mapigano huku ikizitaka pande zote hasimu kuheshimu usitishaji vita uliotangazwa.

Libya inaendelea kushuhudia machafuko na mapigano kati ya makundi hasimu yanayobeba silaha kufuatia mabadiliko yaliyojiri nchini humo mwaka 2011 kufuatia uingiliaji kijeshi wa Marekani na shirika la kijeshi la NATO.../