Meli ya kibiashara ya Ethiopia imetia nanga Eritrea kwa mara ya kwanza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47921-meli_ya_kibiashara_ya_ethiopia_imetia_nanga_eritrea_kwa_mara_ya_kwanza
Meli ya kibiashara ya Ethiopia kwa mara ya kwanza leo imetia nanga nchini Eritrea baada ya kupita miaka 20. Hatua hiyo imejiri kufuatia kusainiwa makubaliano ya kumaliza uhasama kati ya nchi mbili hizo jirani na mahasimu wa zamani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2018 09:25 UTC
  • Meli ya kibiashara ya Ethiopia imetia nanga Eritrea kwa mara ya kwanza

Meli ya kibiashara ya Ethiopia kwa mara ya kwanza leo imetia nanga nchini Eritrea baada ya kupita miaka 20. Hatua hiyo imejiri kufuatia kusainiwa makubaliano ya kumaliza uhasama kati ya nchi mbili hizo jirani na mahasimu wa zamani.

Meli hiyo kwa jina la " Mekele" iliwasili katika bandari ya Massawa katika bahari Nyekundu na inatazamiwa kupakia tani 11,000 za zinc ya Eritrea na kuzisafirisha hadi China. Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa Ethiopia aliahidi kurejesha amani baina ya nchi yake na Eritrea baada ya kula kiapo cha uongozi mwezi Aprili mwaka huu.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed 

Ethiopia imesema inataka kuzifungua tena barabara mbili zinazounganisha nchi hiyo na bandari mbili za Eritrea kama kipaumbele katika mwenendo wa mapatano. Yemane Ghebremeskel Waziri wa Habari wa Eritrea amebainisha kuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia tayari amewasili Eritrea kwa ziara ya kikazi ya siku mbili. Akiwa nchini humo, Abiy atauzuru pia mji wa bandari wa Massawa na mji mkuu Asmara.

Waziri Mkuu wa Ethiopia kwa mara ya kwanza aliitembelea Eritrea mwezi Julai mwaka huu kufuatia makubaliano yaliyofikiwa na nchi mbili jirani ya kumaliza mzozo uliodumu kwa miongo miwili kuhusu hitilafu za mpaka na masuala mengine.