Watu wasiopungua 17 waaga dunia katika ajali ya ndege Sudan Kusini
Watu wasiopungua 17 wamepoteza maisha baada ya ndege ndogo iliyokuwa imebeba abiria kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Juba ikielekea katika mji wa Yirol kuanguka hii leo. Hayo yameelezwa na Taban Abel, Waziri wa Habari wa Sudan Kusini.
Ndege hiyo imeanguka na kuuwa watu 17 na watatu wamejeruhiwa. Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amesema kuwa, ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 22 na kwamba watu wawili hadi sasa hawajulikani walipo. Vilevile miongoni mwa majeruhi waliotambuliwa ni daktari Muitaliano, anayefanya kazi katika taasisi moja isiyo ya serikali, ambaye ametajwa kuwa yuko mahututi na amefanyiwa upasuaji katika hospitali ya Yirol.
Ndege hiyo ilianguka mtoni na watu walioshuhudia wamesema kuwa, miili ya wahanga ilikutwa ndani ya maji huku watoto watatu wakiwa miongoni mwa abiria walioaga dunia.
Ajali kadhaa zimetokea katika miaka ya karibuni katika nchi iliyoathiriwa na vita ya Sudan Kusini. Mwaka jana abiria wanne walijeruhiwa baada ya hali mbaya ya hewa kusababisha ndege waliyokuwa wamepanda kugongana na gari ya zima moto wakati ilipokuwa ikitua na kisha kuwaka moto.