UN yawapongeza mahasimu Sudan Kusini kwa kutia saini mkataba wa amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48129-un_yawapongeza_mahasimu_sudan_kusini_kwa_kutia_saini_mkataba_wa_amani
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa António Guterres amesema kuwa, kusainiwa mkataba ulioboreshwa wa kutatua migogoro nchini Sudan Kusini (RARCSS) tarehe 12 mwezi huu wa Septemba 2018 ni maendeleo mazuri na muhimu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 14, 2018 02:31 UTC
  • UN yawapongeza mahasimu  Sudan Kusini kwa kutia saini mkataba wa amani

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa António Guterres amesema kuwa, kusainiwa mkataba ulioboreshwa wa kutatua migogoro nchini Sudan Kusini (RARCSS) tarehe 12 mwezi huu wa Septemba 2018 ni maendeleo mazuri na muhimu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezipongeza pande zote juu ya hatua hii na amepongeza jitihada za kikanda na kimataifa ambazo zimefanikisha kutiwa saini mkataba huo mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Kupitia taarifa iliyotolewa na naibu msemaji wake mjini New York jana Alkhamisi, Katibu Mkuu wa UN anawataka waliotia saini mkataba huo kuutekeleza kikamilifu ili watu wa Sudan Kusini wapate hatimaye amani wanayostahili.

Guterres amesema, safari bado ina changamoto kubwa na hivyo ni jukumu la jumuiya ya kimataifa kuendelea kufuatilia kwa ukaribu hali ya Sudan Kusini wakati wa utekelezaji wa mapatano hayo.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa António Guterres

 

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake wa kisiasa, Riek Machar siku ya Jumanne walitia saini makubaliano ya amani katika mkutano uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Nchi ya Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Mwezi Disemba mwaka 2013 nchi hiyo changa zaidi duniani ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya Rais Kiir kumtuhumu makamu wake wakati huo, Riek Machar, kuwa alihusika na njama ya kumpindua. Vita hivyo hadi sasa vimeshasababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni wamelazimika kuwa wakimbizi.