UN yalaani kushambuliwa askari wake Sudan Kusini
Kamanda wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini amelaani kitendo cha kushambuliwa maafisa wake nchini humo.
David Shearer amegusia namna ugomvi uliozuka baina ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na wale wa serikali ya Sudan Kusini kiasi kwamba mwanajeshi mmoja wa Sudan Kusini aliamua kufyatua risasi hewani karibu na msafara wa askari wa Umoja wa Mataifa mapema leo Jumapili katika eneo la Yei la kusini mwa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, askari hao wa kulinda amani wamejizuia kuchukua hatua yoyote ya kijeshi kutokana na kuhofia usalama wa raia katika eneo hilo.
Kamanda huyo wa askari wa Umoja wa Mataifa aidha amesema kuwa, wanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini wamefyatua risasi 50 karibu na kambi ya Umoja wa Mataifa katika eneo la Yei na kuitaka serikali ya Juba iwadhibiti wanajeshi wake.
Wakati huo huo mwanajeshi mmoja wa serikali ya Sudan Kusini na askari mmoja wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa raia wa Nepal wameuawa katika mapigano yaliyotokea Juba, mji mkuu wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Hata mapatano ya siku chache zilizopita yaliyotiwa saini Jumatano tarehe 12 mwezi huu wa Septemba mjini Addis Ababa baina ya pande hasimu huko Sudan Kusini inaonekana yamevunjika kwani siku mbili tu baada ya kutiwa saini makubaliano hayo rasmi, pande mbili zimeanza upya kupigana, huku kila upande ukiulaumu upande wa pili kwa kuanzisha mapigano mapya.