Wakazi wa mji mkuu wa Libya, Tripoli walalamikia hali mbaya ya usalama
Wakazi wa mji mkuu wa Libya, Tripoli jana walifanya maandamano wakilalamikia hali mbaya ya usalama katika mji huo mkuu na kutaka kuboreshwa hali ya maisha nchini humo.
Wafanya maandamano hao ambao walikuwa wakipiga nara dhidi ya serikali wamesisitiza kuwa wananchi wa Libya wanakabiliwa na maafa na masaibu mengi na kwamba serikali pia imeshindwa kupunguza mashinikizo yanayowakabili wananchi. Wakazi hao wa Tripoli wametaka kuvunjwa bunge, serikali ya umoja wa kitaifa na baraza la uongozi la nchi hiyo. Aidha wametaka kulindwa raia huko Tripoli na kufurushwa wanamgambo wenye silaha katika mji mkuu huo.
Waandamanaji aidha wametaka kuundwa jeshi na polisi yenye nguvu huko Libya ili kuinusuru nchi na makundi yenye silaha.
Libya ina serikali mbili kufuatia upinzani wa kisiasa ulioko nchini humo. Serikali moja ikiwa ni bunge lenye makao yake katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi na serikali ya umoja wa kitaifa yenye makao yake huko Tripoli. Bunge hilo linaungwa mkono na jeshi la taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar huku serikali ya umoja wa kitaifa chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Fayez al Sarraj ikiungwa mkono na nchi za Magharibi na Marekani.