Watu 100 wauawa na mafuriko nchini Nigeria
Mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini Nigeria yameua watu zaidi ya 100 katika majimbo 10 ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Shirika la Kitaifa la Kushughulikia Majanga NEMA limesema mbali na kusababisha vifo, mafuruko hayo pia yamewalazimisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao katika maeneo ya kusini na katikati mwa nchi, hususan katika majimbo ya Kogi, Niger, Anambra na Delta.
NEMA imesema mito Benue na Niger imevunja kingo zake na kusababisha mafuriko makubwa katika eneo la Lokoja; huku ikiwataka wakazi wa maeneo hayo kuhamia nyanda za juu.
Karibu watu 50 waliaga dunia katika mafuriko mengine katikati ya mwezi Julai mwaka huu nchini Nigeria.
Nigeria iliyoko magharibi mwa bara la Afrika ni miongoni mwa nchi ambazo hukumbwa na mafuriko karibu kila mwaka ambapo mvua kubwa hunyesha nchini humo baina ya mwezi Mei na Septemba.
Mwaka 2012 Nigeria ilikumbwa na mafuriko makubwa katika majimbo 30 kati ya 36 ya nchi hiyo. Mamia ya watu waliaga dunia na wengine milioni mbili kuachwa bila makazi.