Amnesty International: Ukandamiza wa uhuru wa kujieleza Misri umevuka mpaka
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza nchini Misri katika kipindi hiki cha utawala wa Abdel Fattah al Sisi umefikia kiwango cha tahadhari na haujawahi kuonekana nchini humo.
Taarifa iliyotolewa jana na Amnesty International imekosoa mienendo ya kikatili ya askari usalama wa Misri dhidi ya wanaharakati wa masuala ya siasa na kutoa wito wa kuachiwa huru Wamisri waliofungwa jela kwa sababu tu ya kueleza maoni yao kwa njia ya amani.
Amnesty International ambayo imeanzisha kampeni iliyopewa jina la "Misri: Jela ya Wakosoaji", imewataka wafuasi wake kote duniani kuonesha mshikamano wao na Wamisri wanaofungwa jela kwa sababu ya maoni yao na kuitaka serikali ya Cairo ikomeshe kuwatia jela wakosoaji wake.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limetangaza kuwa: "Kuikosoa serikali ya Misri katika kipindi hiki ni hatari sana kuliko kipindi chochote kingine katika historia ya sasa ya nchi hiyo, na serikali ya Abel Fattah al Sisi inakabiliana na Wamisri wanaoeleza maoni yao kwa njia za amani kama wahalifu."
Tangu mwaka 2013 maafisa wa serikali ya Misri waliiweka harakati ya kisiasa na kijamii ya Ikhwanul Muslimin katika orodha ya makundi ya kigaidi na wamezidisha mashinikizo na ukandamizaji dhidi ya viongozi wa harakati hiyo na wanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii.