Makumi ya wafuasi wa Ikhwanul Muslimin wafungwa maisha nchini Misri
Kiongozi wa kundi la Ikhwanul Muslimin la Misri na makumi ya wananchama wa kundi hilo wamehukumiwa kifungo cha maisha jela nchini Misri.
Mtandao wa Intaneti wa al Yaum al Sabii umetangaza habari hiyo leo ukiinukuu hukumu iliyotolewa mahakama ya mkoa ya al Mania inayosema kuwa, Mohammed Badie, mkuu wa Ikhwanul Muslimin na wanachama wengine 64 wa kundi hilo wamehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa tuhuma za kuhusika katika machafuko yaliyotokea katika mji wa el Idwa, mkoani al Mania tarehe 14 Agosti 2013.
Hukumu ya kifungo cha maisha dhidi ya Mohammed Badie imetolewa katika hali ambavyo hivi karibuni pia mahakama ya rufaa ya Cairo ilimuhukumu kifungo cha maisha jela kwa kumuhusisha na kesi ya mgomo na kukusanyika wafuasi wa Mohamed Morsi katika medani za ,Rabia al Adawiya na al Nahdha mjini humo baada ya rais huyo wa zamani wa Misri kupinduliwa na jeshi mwaka 2013.
Vile vile mahakama ya rufaa ya Cairo imewahukumu kifo wafuasi wengine 75 wa Ikhwanul Muslimin kwa kuhusika na machafuko ya mwaka 2013 na kuwahukumu wafuasi wengine 46 wa kundi hilo kifungo cha maisha jela.
Tarehe 14 Agosti 2013, rais wa hivi sasa wa Misri, Abdel Fattah el Sisi ambaye alikuwa waziri wa ulinzi wakati huo, alitoa amri ya kushambuliwa wafuasi wa Mohamed Morsi mjini Cairo na kuua na kujeruhi mamia ya watu.
Mwaka 2013, viongozi wa Misri waliiweka Ikhwanul Muslimin katika orodha ya makundi ya kigaidi na wamekuwa wakichukua hatua kali dhidi ya wafuasi wa kundi hilo.