Mahkama ya Misri yakataa pendekezo la kufanya maridhiano na dikteta Mubarak
Vyombo vya Mahkama nchini Misri vimetupilia mbali pendekezo la kuridhiana na dikteta aliyeuzuliwa madarakani Hosni Mubarak, pamoja na watoto wake.
Jumapili ya jana Mahakama ya rufaa ya Misri ilipinga pendekezo la Mubarak pamoja na watoto wake Alaa na Gamal kwa ajili ya kuridhiana katika faili la kuiba fedha za nchi hiyo katika ikulu ya rais kipindi akiongoza nchi hiyo. Mwezi Mei 2016 mahakama ya Misri ilimuhukumu Hosni Mubaraka pamoja na watoto wake kifungo cha miaka mitatu na kutakiwa kurejesha fedha sawa na Pauni milioni 125 za Misri, sawa na Dola milioni saba na kadhalika kulipa faini ya Pauni milioni 21. Baada ya kutolewa hukumu hiyo, Mubarak na watoto wake walitoa pendekezo kwa mahakama hiyo la kufanya maridhiano, hatua ambayo kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo, lau kama ingekubaliwa, basi faili hilo lingefungwa huku matokeo yake ikiwa ni pamoja na kuhitimishwa marufuku ya miaka mitano kwa watuhumiwa wa faili hilo kuingia katika ulingo wa kisiasa.
Mubarak na watoto wake Alaa na Gamal walitiwa mbaroni mwezi April 2011 baada ya mwamko wa wananchi. Aidha mwezi Machi 2017 dikteta huyo aliyeiongoza Misri kwa miongo mitatuu kwanza alifutiwa mashtaka na kisha kuachiliwa huru huku watoto wake nao wakiachiliwa huru mwezi Oktoba mwaka huo huo ingawa hadi sasa faili lao la kuiba fedha za serikali limeendelea kubakia wazi. Katika faili hilo, Mubarak na watoto wake wanakabiliwa na kuiba zaidi ya Pauni milioni 125 kutoka katika bajeti maalumu ya ikulu ya rais.