Mripuko wa kipindupindu waua watu 67 nchini Niger
(last modified Thu, 27 Sep 2018 15:46:12 GMT )
Sep 27, 2018 15:46 UTC
  • Mripuko wa kipindupindu waua watu 67 nchini Niger

Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa, watu wasiopungua 67 wamepoteza maisha kutokana na mripuko wa kipindupindu nchini Niger tokea mwezi Julai mwaka huu hadi sasa.

Taarifa iliyotolewa leo Alkhamisi na Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema kuwa, vifo 55 vilivyotokana na maradhi hayo vimeripotiwa katika mji wa Maradi, ambao umenakili kesi 3,232 kufikia sasa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Niger, maeneo mengine yaliyoathirika zaidi na mripuko huo ni Dosso lililoko kusini mwa nchi, Tahoua upande wa magharibi na eneo lililoko katikati mwa nchi la Zinder.

Waathiriwa kipindupindu waliolazwa hospitalini nchini Nigeria

Haya yanajiri siku chache baada ya UN kutangaza kwamba, watu karibu 200 wamepoteza maisha kutokana na kipindupindu katika nchi jirani ya Nigeria, huku kesi zaidi ya 3,100 za ugonjwa huo zikirekodiwa kufikia sasa katika majimbo 12 ya nchi hiyo hususan Yobe na Borno.

Kipindupindu ni ugonjwa hatari unaosababishwa na bakteria hasa katika utumbo mwembamba, na husambaa kupitia maji au vyakula vilivyochafuliwa na wadudu kama vile nzi.

Tags