Mapigano yaanza upya mjini Tripoli, Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48469-mapigano_yaanza_upya_mjini_tripoli_libya
Vyombo mbalimbali vya habari vimetangaza kuwa, utulivu katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, haukudumu ila kwa siku chache tu kwani tayari mapigano yameanza upya mjini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 29, 2018 15:24 UTC
  • Mapigano yaanza upya mjini Tripoli, Libya

Vyombo mbalimbali vya habari vimetangaza kuwa, utulivu katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, haukudumu ila kwa siku chache tu kwani tayari mapigano yameanza upya mjini humo.

Gazeti la al Hayat limezinukuu duru za kuaminika zikisema kuwa, baada ya kupita siku chache za utulivu na kusimamishwa mapigano nchini Libya, mapigano hayo yameanza upya leo Jumamosi katika eneo la Warshefana.

Duru nyingine ya kuaminika imesema kuwa, mapigano hayo yamezuka baina ya brigedi za Osama al Juaili na wanamgambo wa Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mapigano ya hivi karibuni yamepelekea watu 115 kuuawa na 400 wengine kujeruhiwa mjini Tripoli

 

Hivi karibuni viongozi wa Libya walitangaza habari ya kufikiwa makubaliano ya kusimamisha mapigano baada ya karibu mwezi mzima wa vita baina ya makundi yenye silaha mjini humo.

Karibu mwezi mmoja nyuma, mji mkuu wa Libya ulikumbwa na mapigano baina ya wanamgambo wenye mfungamano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kundi linalojiita Brigedi ya al Liwaa al Saab'i. Mapigano hayo yalisimamishwa siku chache zilizopita baada ya kupelekea watu 115 kuuawa na karibu 400 wengine kujeruhiwa.

Tangu mwaka 2011, Libya haijawahi kuwa na utulivu wa angalau siku moja, baada ya Marekani na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika kampeni ya kumg'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi.