Algeria: Afrika imedhulumika katika Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48481-algeria_afrika_imedhulumika_katika_umoja_wa_mataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema, Afrika imedhulumika katika Umoja wa Mataifa na kwenye Baraza la Usalama la umoja huo na kwa hivyo dhulma hiyo inapasa iondolewe.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Sep 30, 2018 04:14 UTC
  • Algeria: Afrika imedhulumika katika Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema, Afrika imedhulumika katika Umoja wa Mataifa na kwenye Baraza la Usalama la umoja huo na kwa hivyo dhulma hiyo inapasa iondolewe.

Abdelkader Messahel ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa kwa niaba ya nchi yake kwenye kikao cha 73 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo jana na akaeleza kwamba: Umoja wa Mataifa inapasa pawe mahali pa mazungumzo kati ya mataifa ya dunia na pa kulindwa haki za mataifa yote, lakini taasisi hiyo ya kimataifa hivi sasa inahitaji mageuzi katika muundo na mfumo wake wa utendaji kazi hususan katika Baraza la Usalama.

Messahel ameongeza kuwa: Katika utekelezaji wa marekebisho hayo inapasa dhulma ya kihistoria liliyofanyiwa bara la Afrika ihitimishwe kwa sababu Afrika haina uwakilishi wa kutosha katika Baraza la Usalama na kwamba kwa kufanya mageuzi yanayotakikana, Umoja wa Mataifa unaweza kurejesha tena itibari yake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amezungumzia pia matukio ya kieneo katika Mashariki ya Kati na Afrika na kueleza kwamba nchi zote zinapaswa kufanya juhudi za kulinda mamlaka ya kujitawala, uhuru na umoja wa ardhi za mataifa, ambapo kuhusiana na hali ya mambo katika nchi za Mali, Libya, Syria na Yemen amesisitiza kuwa, kuna ulazima wa amani na uthabiti kurejeshwa katika nchi hizo ili kazi ya ukarabati na ujenzi mpya ianze mara moja.

Kikao cha 73 cha Baraza Kuu la UN kikiwa kinaendelea mjini New York

Kuhusiana na kadhia ya Palestina, Abdelkader Messahel amesema, Algeria inaamini kwamba ni haki ya wananchi wa Palestina kuwa na nchi yao huru, mji mkuu wake ukiwa ni Baitul Muqaddas (Jerusalem) na kwamba endapo lengo hilo litafikiwa kunaweza kuwepo matumaini ya kuhitimishwa mapigano ya miongo saba katika Mashariki ya Kati.

Hotuba za viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kikao cha 73 cha Baraza Kuu la umoja huo zilianza kutolewa tarehe 25 Septemba na zitaendelea hadi tarehe Mosi ya mwezi ujao wa Oktoba katika Makao Makuu ya umoja huo mjini New York.../