Saudia, Imarati na Marekani kuunda muungano wa kijeshi Pembe ya Afrika
(last modified Mon, 01 Oct 2018 03:33:05 GMT )
Oct 01, 2018 03:33 UTC
  • Saudia, Imarati na Marekani kuunda muungano wa kijeshi Pembe ya Afrika

Gazeti moja la nchini Qatar limefichua kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kushirikiana na Saudi Arabia zina nia ya kuunda muungano mwingine wa kijeshi wa nchi kadhaa katika eneo la Pembe ya Afrika.

Gazeti la al Sharq la nchini Qatar limefichua kuwa, Imarati imetoa pendekezo la kuundwa muungano wa kijeshi utakaozishirikisha pia Misri, Ethiopia, Eritrea na Saudia kwa lengo la kulinda usalama wa Bahari Nyekundu.

Gazeti hilo limesema, muungano huo mpya ni sehemu ya mpango wa Marekani wa kuingilia masuala ya eneo la Pembe ya Afrika.

Wanajeshi wa Imarati

 

Viongozi wa serikali ya Djibouti nao wamefichua kuwa, kwa muda sasa Imarati imekuwa ikifuatilia kuanzisha vituo vyake vya kijeshi katika eneo hilo kwa kushirikiana na Saudia na kwa msaada wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ripoti hiyo imetolewa katika hali ambayo uhusiano wa Imarati na baadhi ya nchi za Pembe ya Afrika umezidi kuharibika katika miezi ya hivi karibuni.

Uhusiano wa Djibouti na Abu Dhabi umekumbwa na migogoro baada ya ndege moja ya kijeshi ya Umoja wa Falme za Kiarabu kutua katika kambi ya kijeshi ya Djibouti bila ya idhini ya viongozi wa nchi hiyo.

Baada ya kitendo hicho cha Imarati cha kutoheshimu haki ya kujitawala Djibouti, kulizuka mashambulizi makali ya maneno baina ya viongozi wa nchi hizo mbili na Djibouti ikawafukuza nchini humo askari wa Imarati na zana zao za kijeshi.

Tags