Majaji wa mahakama ya ICC wasikiliza kesi ya Gbagbo
Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) leo wamesikiliza matakwa ya Rais wa zamani wa Ivory Coast anayekabiliwa na kesi ya kufanya jinai dhidi ya binadamu ambaye ametaka kesi hiyo ifungwe kutokana na kukosekana ushahidi dhidi yake.
Mawakili wa Laurent Gbagbo wamesema katika waraka wao uliosomwa mahakamani kwamba wendesha mashtaka wameshindwa kutoa ushahidi wa kutosha wa kuunga mkono madai yao.
Hata hivyo waendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wamesema Gbagbo anayekabiliwa na kesi nne za kufanya jinai dhidi ya binadamu ana kesi ya kujibu.
Naibu Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya ICC, James Steward amesema kwamba kuna ushahidi unaoweza kuthibisha uhalifu uliofanywa na rais wa zamani wa Ivory Coast.
Laurent Gbagbo anayeshikiliwa The Hague huko Uholanzi anakabiliwa na mashtaka ya kutenda jinai kadhaa ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji, mateso na vitendo vingine vya kinyama ambavyo vilifanyika baada ya uchaguzi wa 2010 wakati Gbagbo alipokataa kukubali kushindwa na mpinzani wake, Alassane Ouattara.
Hatua hiyyo ya Gbagbo na waungaji mkono wake iliituumbukiza Ivory Coast katika machafuko makubwa yaliyopelekea kuuawa maelfu ya raia wasio na hatia.