Wanigeria waandamana, waitaka serikali imwachie huru Sheikh Zakzaky
Wananchi wa Nigeria wamefanya tena maandamano makubwa mjini Abuja wakitaka kuachiwa huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo, Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Waandamanaji hao wamelaani kitendo cha serikali ya Nigeria cha kuendelea kumshikiliwa jela Sheikh Zakzaky na mkewe licha ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo kutaka aachiwe huru haraka iwezekanavyo.
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walikamatwa tarehe 13 Disemba mwaka 2015 katika shambulizi lililofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya nyumba yake na kituo cha Kiislamu katika mji wa Zaria kwenye jimbo la Kaduna huko kaskazini mwa Nigeria.
Katika shambulizi hilo jeshi la Nigeria liliwapiga risasi na kuwaua shahidi mamia ya Waislamu wa mji huo wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky.
Disemba mwaka 2016 Mahakama Kuu ya Nigeria iliiamuru serikali ya nchi hiyo kumwachia huru mwanazuoni huyo wa Kiislamu na kulitaka jeshi na vyombo vya usalama vya nchi hiyo kulipa fidia ya dola laki moja na nusu kwa familia yake. Hata hivyo hadi sasa serikali ya Nigeria imekataa kutekeleza uamuzi huo wa mahakama.
Duru za kuaminika zinasema hali ya kimwili ya Sheikh Zakzaky ni mbaya sana na zimetoa wito achiwe huru mara moja.