Wafungwa Sudan Kusini wadhibiti seli katika mji mkuu Juba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48645-wafungwa_sudan_kusini_wadhibiti_seli_katika_mji_mkuu_juba
Wafungwa kadhaa jana Jumapili waliwapokonya silaha walinzi na kisha kudhibiti eneo moja la seli ya wafungwa huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini. Hayo yameelezwa na Idara ya Usalama wa taifa ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 07, 2018 23:04 UTC
  • Wafungwa Sudan Kusini wadhibiti seli katika mji mkuu Juba

Wafungwa kadhaa jana Jumapili waliwapokonya silaha walinzi na kisha kudhibiti eneo moja la seli ya wafungwa huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini. Hayo yameelezwa na Idara ya Usalama wa taifa ya nchi hiyo.

Imeongeza kuwa mvutano ulianza wakati mfungwa mmoja kwa jina la Kapteni Keribino Wol alipomzidi nguvu mlinzi katika lango la kuingilia kizuizi kilichopo katika makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa ya Sudan Kusini katika jengo la Blue House na kisha akamnyang'anya silaha aliyokuwa nayo.

Kapteni Keribino Wol 

Kapteni Wol aliliambia shirika la habari la Reuters akiwa kizuizini hapo kuwa, wamechoka na sasa wameamua kudhihirisha upinzani wao kwa kukosekana uadilifu na ukandamizaji uliopo. Kapteni Keribino Wol alitiwa mbaroni mwezi Aprili na hadi sasa hajawahi kufikishwa mahakamani. Amesema wafungwa wote wa kisiasa na wale wanaoshikiliwa wanahitaji kuachiwa huru haraka iwezekanavyo au kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria. Amesema kushindwa wafungwa kufikishwa mahakamani ni kinyume cha sheria. 

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013 wakati hali ya mzozo kati ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo na aliyekuwa Makamu wake Riek Machar iliposhtadi na kuibua mapigano baina ya wafuasi wa pande mbili hizo.