Ajali ya basi yaua 50 Kenya, kuna uwezekano idadi ikaongezeka
Watu wasiopungua 50 wameaga dunia katika ajali ya basi iliyotokea mapema leo ikiwa njiani kuelekea Kisumu kutoka Nairobi.
Ajali ya basi hilo linalomilikiwa na Western Express Sacco imetokea katika barabara ya Londiani-Muhoroni.
Basi hilo lenye viti vya abiria 67 liliacha njia katika mteremko mkali na kubimbirika umbali wa mita ishirini kutoka barabarani.
Kamanda wa Polisi ya Kaunti ya Kericho, James Mogera amesema idadi ya wahanga wa ajali hiyo yumkini ikaongezeka kutokana na kwamba, baadhi ya abiria wa basi hiyo wangali wamenasa katika mabaki yake.
Majeruhiwa wa ajali hiyo wamepelekwa katika zahanati ya Fort Ternan na hospitali ya Muhoroni kwa ajili ya matibabu.
Watoto 8 wenye umri wa chini ya miaka mitano ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo.