Watu 31 waaga dunia katika maporomoka ya ardhi Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48739-watu_31_waaga_dunia_katika_maporomoka_ya_ardhi_uganda
Makumi ya watu wameripotiwa kupoteza maisha katika maporomoko ya ardhi yaliyotokea jana adhuhuri katika vijiji vilivyoko kwenye kaunti ndogo ya Bakalasi, wilayani Bududa mashariki mwa Uganda.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 12, 2018 04:03 UTC
  • Watu 31 waaga dunia katika maporomoka ya ardhi Uganda

Makumi ya watu wameripotiwa kupoteza maisha katika maporomoko ya ardhi yaliyotokea jana adhuhuri katika vijiji vilivyoko kwenye kaunti ndogo ya Bakalasi, wilayani Bududa mashariki mwa Uganda.

Martin Owor, Kamishna wa Idara ya Kupambana na Majanga nchini humo amesema watu 31 wamethibitishwa kupoteza maisha, baada ya maporomoko ya ardhi kutokea chini ya Mlima Elgon, mashariki mwa Uganda.

Mkuu wa Polisi katika eneo la Elgon, Manshur Sowedi hapo jana alisema watu 20 wameaga dunia katika maporomoko hayo na kwamba yumkini idadi hiyo ikaongezeka.

Mashuhuda na manusura wa janga hilo wanasema walioaga dunia ni zaidi ya watu 50 na kwamba makumi ya wengine waliopata majeraha wanatibiwa katika Kituo cha Afya cha Bukalasi.

Duru za habari zimeripoti kuwa, miongoni mwa watu waliofariki dunia katika janga hilo ni wanafunzi wa shule ya chekechea ya Suume Junior Academy.

Mafuriko Uganda

Viongozi wa eneo hilo wamesema watu zaidi ya 500 wamelazimika kuyahama makazi yao kufuatia maporomoko hayo, na kwamba wanahitaji msaada wa dharura wa chakula na malazi.

Mvua kubwa iliyonyesha kwa takriban masaa manne hiyo jana ilipelekea Mto Suume kuvunja kingo zake na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika eneo hilo, lililoko umbali wa kilomita 150 toka mji mkuu Kampala