Oct 13, 2018 15:56 UTC
  •  Hassan Wario
    Hassan Wario

Waziri wa zamani wa michezo wa Kenya atapandishwa kizimbani kujibu mashtaka ya kupora fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya wanariadha wa nchi hiyo walioshiriki michezo ya Olimpiki nchini Brazil miaka miwili iliyopita.

Uchunguzi uliofanyika umempata Hassan Wario aliyekuwa waziri wa michezo wa Kenya na maafisa wengine watano na kesi ya kujibu kuhusu tuhuma za kupora fedha za wanariadha katika michezo hiyo.

Mkuu wa Mashtaka ya Umma wa Kenya, Noordin Haji amesema maafisa hao wa zamani wanakabiliwa na mashtaka kumi yanayohusiana na utumiaji mbaya wa madaraka yao na kutotekeleza sheria.

Hassan Wario ambaye ameteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini Austria hakuweza kupatikana mara moja kutoa maelezo. Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Kipchoge Keino ambaye alikuwa mkuu wa Kamati ya Taifa ya Olimpiki.

Noordin Haji amesema Wario na wenzake wanakabiliwa na tuhuma zinazohusiana na kupotea kwa shilingi zaidi ya milioni 55 zilizotengwa kwa ajili ya wanariadha wa Kenya katika michezo ya Olimpiki ya Rio miaka miwili iliyopita.

Makumi ya maafisa wa ngazi za juu katika serikali ya Kenya wanakabiliwa na tuhuma za ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma ikiwa ni katika harakati za Rais Uhuru Kenyatta za kukabiliana na ufisadi zilizoanza mwezi Mei mwaka huu.  

Kenya ilipata mafanikio makubwa katika michezo ya Olimpiki ya Rio kwa kushinda medali 6 za dhahabu, sita za fedha na moja ya shaba lakini mafanikio hayo yalifunikwa na madai ya ufisadi unaosemekana kufanywa na maafisa wa ngazi za juu serikalini na wasimamizi wa timu ya taifa ya Olimpiki.  

Tags