Watu 75 watekwa nyara Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu
Serikali ya Tanzania imesema kuwa, watu wapatano 75 wametekwa nyara katika nyakati na maeneo tofauti nchini humo kwenye kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Kangi Lugola amesema kuwa, licha ya matukio hayo lakini usalama ni imara nchini humo.
Kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania imetolewa siku tatu tangu alipotekwa mfanyabiashara bilionea Mohammed Dewji. Jeshi la polisi la Tanzania linaendelea na msako wa kumtafuta bilioni huyo.
Akiwathibitishia waandishi wa habari kwamba serikali ya Tanzania inalifuatilia kwa nguvu suala hilo, Waziri Lugola amesema amefanya kikao na Mkuu wa Polisi nchini humo na kutafakari hali ya uhalifu nchini humo.
Amesema licha ya polisi wa nchi hiyo kufanya juhudi kubwa za kulinda usalama wa raia, lakini mwaka 2016 kulikuwa na matukio ya watu 9 kutekwa ambapo watano walipatikana wakiwa hai kwa ushirikiano na wananchi.
Vile vile amesema, mwaka jana 2017, watu 27 walitekwa nyara, na polisi walifanikiwa kuwapata 22 wakiwa hai na wawili wakiwa wamekufa, huku watatu hawakupatikana.
Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania, katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba 11, 2018, watu 21 wametekwa nyara nchini humo ambapo 17 kati yao wamepatikana wakiwa hai na wanne hawajapatikana hadi hivi sasa.
Pia amesema, watoto 18 wametekwa nchini humo tangu mwaka 2016 hadi hivi sasa, 15 kati yao wamepatikana wakiwa hai, wawili wakiwa wamekufa na mmoja hajapatikana hadi hivi sasa.
Aidha amesema, miongoni mwa sababu za vitendo hivyo vya utekaji nyara ni za kisiasa, kiuchumi, kulipiza kisasi, wivu wa mapenzi na ushirikina.