Oct 21, 2018 14:43 UTC
  • Waasi wa ADF waua 13 na kuteka watoto 12 Beni, Kongo DR

Waasi wa Uganda wa ADF-Nalu wamefanya tena mashambulio dhidi ya ngome za jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuua watu 13 mbali na kuwateka nyara watoto wasiopungua 12.

Ofisa wa ngazi za juu wa jeshi la Kongo DR ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, waasi hao mbali na kushambulia vituo vya kijeshi, lakini pia walivamia makazi ya raia katika mji wa Beni, mkoa wa Kivu Kaskazini kuanzia jana Jumamosi hadi mapema leo Jumapili.

Wakazi wa Beni mapema wameandamana huku wakiwa wamebeba miili ya baadhi ya watu waliouawa na waasi wa ADF na kuipeleka nje ya ofisi ya Baraza la Mji wakilalamikia kushtadi mauaji dhidi yao. Hata hivyo maafisa wa polisi wametumia mabomu ya kutoa machozi kutawanya maandamano hayo.

Tarehe 22 Septemba pia raia 14 na wanajeshi 4 wa serikali ya Kongo DR  waliuawa katika shambulio lililodaiwa kufanywa na waasi wa Uganda wa ADF, mwezi mmoja baada ya genge hilo kufanya mashambulio mengine katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC na kuua watu sita.

 

Wakazi wa Beni wakiandamana kulalamikia usalama duni katika mji huo

Kwa mujibu wa watetezi wa watoto nchini DRC, watoto 34 waliuawa huku wengine zaidi ya 215 wakitekwa nyara na magenge ya waasi katika mkoa wa Kivu Kaskazini mwaka jana pekee. 

Waasi wa Uganda wa ADF walianzisha harakati zao mashariki mwa Kongo tangu mwaka 1994 na katika miaka hiyo yote wameuwa mamia ya raia wa eneo hilo.

 

Tags