Misri yatangaza kurefusha muda wa hali ya hatari kwa miezi 3 mingine
Bunge la Misri jana lilipiga kura ya kurefusha muda wa hali ya hatari kwa miezi mingine mitatu na hivyo kurefusha nguvu ya serikali ya kutumia madaraka maalumu kuelekea mwaka 2019.
Kwa mara ya kwanza Misri ilianza kutekeleza hali ya hatari nchini mwezi Aprili mwaka 2017 baada ya kutokea milipuko katika makanisa mawili na kuuawa watu wasiopungua 45; na baadaye ikaongeza muda wa hali hiyo kwa miezi mingine mitatu.
Tangazo hili la kuongeza muda wa hali ya hatari uliopigiwa kura na bunge hiyo jana unahitajia kuidhinishwa na bunge katika kipindi cha siku saba. Hali hii ya hatari inatoa mwanya kwa askari usalama kuchukua hatua zinazohitajika kukabiliana na hatari, ufadhili kwa makundi ya kigaidi na pia kudhamini usalama katika maeneo yote ya nchi.
Hali ya hatari nchini Misri inawapatia maafisa husika madaraka makubwa ya kuwatia mbaroni na kuwadhibiti wale wanaotajwa kuwa ni maadui wa nchi. Vikosi vya usalama vya Misri vimekuwa vikipambana na oparesheni za wanamgambo magaidi wenye ngome zao katika eneo la Sinai ya kaskazini. Mwezi Februari mwaka huu jeshi la Misri lilianzisha oparesheni kubwa ya kuwasaka wanamgambo hao magaidi.