Misri yajiandaa kutuma jeshi nchini Libya
(last modified Mon, 22 Oct 2018 14:49:39 GMT )
Oct 22, 2018 14:49 UTC
  • Misri yajiandaa kutuma jeshi nchini Libya

Duru za habari zimetangaza kuwa, serikali ya Misri imechukua uamuzi wa kutuma jeshi katika nchi jirani ya Libya kwa ajili ya kulisaidia jeshi la Khalifa Haftar linalojulikana kama Jeshi la Taifa.

Mtandao wa gazeti la al Rai al Youm umevinukuu vyombo vya jeshi la Misri vikitangaza kuwa, Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo na kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya, Jenerali Khalifa Haftar wamefikia mapatano ya kushirikiana kijeshi chini ya upatanishi wa Imarati. 

Mtandao huo umeongeza kuwa, kuna uwezekano kwamba, Rais wa Misri, Jenerali al Sisi atatuma Libya idadi kubwa ya kikosi maarufu cha jeshi cha al Saiqah. Inasemekana pia kwamba, Saudi Arabia na Imarati zinaunga mkono suala la kutumwa majeshi ya Misri nchini Libya. 

Wakati huo huo habari zinasema maafisa wa jeshi la Khalifa Haftar tangu Jumatano iliyopita wamekuwa wakifanya mazungumzo na wawakilishi wa taasisi za upelelezi na jeshi la Misri. 

Jeshi la Misri.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetahadharisha kuhusu vikao na mazungumzo hayo na kutangaza kuwa, kambi ya Haftar imekuwa ikikutana na kufanya mazungumzo yanayotia shaka na Misri ambayo inapendelea upande mmoja katika mgogoro wa ndani wa Libya. 

Baadhi ya weledi wa mambo wanasema Misri inashirikiana na Marekani na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO katika ushirikiano wake na kambi ya Khalifa Haftar.    

Tags