Ethiopia yasaini makubaliano ya amani na kundi la waasi wa Ogaden
(last modified Tue, 23 Oct 2018 03:02:46 GMT )
Oct 23, 2018 03:02 UTC
  • Ethiopia yasaini makubaliano ya amani na kundi la waasi wa Ogaden

Ethiopia imesema kuwa imesaini makubaliano ya amani na kundi lililokuwa likipigania kujitenga la Waasi wa Harakati ya Taifa ya Ukombozi wa Ogaden (ONLF) na hivyo kuhitimisha rasmi uasi uliodumu kwa zaidi ya miongo mitatu katika mkoa wa Somalia mashariki mwa nchi hiyo.

Harakati hiyo ambayo iliasisiwa mwaka 1984 imekuwa ikipigania haki ya kujitawala ya watu wa kabila la Wasomali wanaoishi mashariki mwa Ethiopia ikiwemo kujitenga. Workneh Gebeyehu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia na Makamu wa Rais wa mkoa wa Somalia Mustafa Omer walielekea Asmara mji mkuu wa Eritrea kwa ajili ya kusaini makubaliano ya amani na harakati ya ONLF.

Ujumbe wa serikali ya Ethiopia na wa harakati hiyo ya waasi walikuwa na majadiliano yaliyozaa matunda na kupelekea kufikiwa makubaliano hayo ya kihistoria yanayoiruhusu harakati hiyo ya waasi kuendesha mapambano ya kisiasa kwa njia ya amani. Tangu aingie madarakani mwezi Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amewaachia wafungwa wa kisiasa na kutoa kipaumbele kwa suala la kufikiwa mapatano na makundi mbalimbali ya nchi hiyo.