Mazungumzo ya amani ya Burundi yanafanyika leo, serikali ya Bujumbura haishiriki
(last modified Wed, 24 Oct 2018 08:05:50 GMT )
Oct 24, 2018 08:05 UTC
  • Mazungumzo ya amani ya Burundi yanafanyika leo, serikali ya Bujumbura haishiriki

Duru ya tano ya mazungumzo ya amani ya Burundi yanayosimamiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inaanza kufanyika leo mjini Arusha kaskazini mwa Tanzania.

Mpatanishi wa mazungumzo hayo ya amani ya Burundi, Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa, anatarajiwa kuzikutanisha pande zinazohasimiana  katika mazungumzo ambayo yanatajwa kuwa, huenda yakawa ni ya mwisho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mazungumzo hayo yatakayoendelea hadi tarehe mwezi huu yanatarajiwa kujikita katika kusaka muafaka kuhusu namna bora itakayosadia pande hizo kushiriki kwa uhuru na uwazi katika maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2020.

Benjamin William Mkapa, mjumbe maalumu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika mazungumzo ya amani ya Burundi

Wakati mazungumzo ya amani kuhusu Burundi yakifanyika leo mjini  Arusha nchini Tanzania, tayari yameingia dosari baada ya serikali ya Bujumbura, pamoja na vyama washirika, kutangaza kuwa haviatashiriki duru hii ya mazungumzo.

Serikali ya Burundi inasema haitaweza kushiriki katika mazungumzo hayo kwa kuwa nchi hiyo iko katika maombolezo ya mwezi mzima kuwakumbuka mashujaa wa taifa hilo kwa mujibu wa Evariste Ndayishimiye Katibu Mkuu wa chama tawala cha CNDD-FD.

Kwa upande wao muungano wa upinzani wa ndani ya Burundi “AMIZERO YA BARUNDI” unaoongozwa na Agathon Rwassa, umeeleza kushangazwa na hatua ya Serikali, ukisema serikali ya Rais Nkurunziza inatafuta sababu ili kukwepa mazungumzo ya Arusha.

Tangu mazungumzo ya amani ya Burundi yaanze Disemba 2015 hadi sasa hakujapigwa hatua yoyote ya maana, huku wapinzani wakiituhumu serikali ya Bujumbura kwamba, haina nia ya dhati ya kuhakikisha mazungumzo hayo yanakuwa na natija inayofaa.