Ethiopia yaondoa rasmi viza kwa Waafrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49072-ethiopia_yaondoa_rasmi_viza_kwa_waafrika
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed jana alitangaza kuwa, kuanzia tarehe 9 mwezi ujao wa Novemba, nchi yake itawaondolea viza raia wote wa nchi za Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 27, 2018 04:04 UTC
  • Ethiopia yaondoa rasmi viza kwa Waafrika

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed jana alitangaza kuwa, kuanzia tarehe 9 mwezi ujao wa Novemba, nchi yake itawaondolea viza raia wote wa nchi za Afrika.

Vyombo vya habari vya Ethiopia vimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Abiy Ahmed anaamini kwamba nchi za Afrika zinapaswa kukurubiana na kushirikiana zaidi kiuchumi na kiutamaduni.

Abiy Ahmed ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza Muislamu katika historia ya Ethiopia amekuwa akifanya mabadiliko makubwa ambayo yanahesabiwa kuwa ni sawa na mapinduzi ya kisiasa nchini humo. Hadi hivi sasa ameshachukua hatua muhimu sana kwa ajili ya wananchi wa Ethiopia na majirani zao kama Eritrea ambayo kabla ya kuingia kwake madarakani ilikuwa adui mkubwa wa Ethiopia.

 

Waziri Mkuu huyo wa Ethiopia amejenga uhusiano mzuri baina ya nchi yake na Eritrea baada ya kuirejeshea nchi hiyo ardhi zake zilizokuwa zinakaliwa kwa nguvu na Ethiopia.

Wiki iliyopita pia alilifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri na nusu ya wizara zake yaani wizara 10 amewapa wanawake. Hatua hiyo ni ya aina yake si barani Afrika tu, bali dunia nzima.