Jeshi la Misri laua magaidi 13 katikati mwa nchi hiyo
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imetangaza kwamba maafisa wa usalama wa nchi hiyo wamewaua wanachama 13 wa kundi moja la kigaidi katikati ya nchi.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema kuwa magaidi hao walikuwa wamejificha katika eneo la Asyut na Kharga Oasis yaliyoko kilometa 450 kusini mwa mji mkuu Cairo, na kwamba maafisa usalama walipambana nao na kupelekea 13 kati ya magaidi hao kuuawa. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri pia imetangaza kwamba magaidi wamekuwa wakitoa mafunzo ya utumiaji silaha na kutega mabomu kwa wanachama wapya wanaojiunga na makundi ya kigaidi. Hii ni katika hali ambayo Jumatano iliyopita maafisa usalama wa Misri waliwaua magaidi wengine 11 katika mkoa wa Asyut.
Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita jeshi la Misri limekuwa likiendesha mapambano mengi dhidi ya magaidi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo hususan katika mkoa wa Sinai kaskazini, mapigano ambayo hadi sasa yanaendelea. Katika uwanja huo, jeshi la Misri na kwa amri ya Rais Abdel Fattah el-Sisi lilianzisha operesheni kabambe dhidi ya wanamgambo wanaobeba silaha ambapo kwa mujibu wa ripoti rasmi hadi sasa zaidi ya magaidi 200 wamekwisha uawa katika kipindi hicho.