Guterres alaani kuuawa askari wa Umoja wa Mataifa nchini Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49096-guterres_alaani_kuuawa_askari_wa_umoja_wa_mataifa_nchini_mali
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali mauaji dhidi ya askari wa kusimamia amani wa umoja huo katika nchi ya magharibi mwa Afrika ya Mali.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 28, 2018 12:06 UTC
  • Guterres alaani kuuawa askari wa Umoja wa Mataifa nchini Mali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali mauaji dhidi ya askari wa kusimamia amani wa umoja huo katika nchi ya magharibi mwa Afrika ya Mali.

Stephane Dujarric, msemaji wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika taarifa maalumu kwamba, umoja huo unalaani vikali kuuawa askari wake wa kusimamia amani huko nchini Mali.

Mbali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kulaani mauaji hayo sambamba na kuwapa pole familia zilizopoteza ndugu zao amesisitiza azma ya umoja huo ya kurejesha amani na usalama katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Askari wawili wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA) waliuawa baada ya kuviziwa na kushambuliwa ghafla na genge moja la kigaidi katikati mwa nchi hiyo.

Askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA)

Taarifa ya MINUSMA imesema kuwa, katika hujuma hiyo ya jana Jumamosi ya magaidi dhidi ya kambi ya askari hao wa UN katika mji wa Ber, karibu na jiji la Timbuktu, eneo la Mopti, wanajeshi wengine watano walijeruhiwa.

Nchi ya Mali ilikumbwa na ghasia na ukosefu wa amani baada ya mapinduzi yaliyotokea nchini humo mwaka 2012. 

Mwaka mmoja baadaye, Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MINUSMA) na wanajeshi wa Ufaransa walitumwa nchini humo kwa ajili ya kuwadhaminia usalama raia, lakini vikosi hivyo havijakuwa na utendaji wa kuridhisha katika kurejesha utulivu nchini humo huku vitisho vya ugaidi vikiendelea kuitatiza nchi hiyo.