Sudan Kusini yawaachia huru msemaji na mshauri wa kiongozi wa waasi
Sudan Kusini leo imewaachia huru kutoka jela msemaji na mshauri wa Riek Machar kiongozi wa waasi wa nchi hiyo. Hayo yameelezwa na afisa wa serikali ya Juba.
Jumatano iliyopita Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini aliagiza kuachiwa huru Kanali William Endley aliyekuwa mshauri wa Riek Machar ambaye ni raia wa Afrika Kusini na msemaji wake James Gatdet, ikiwa ni katika kuimarisha makubaliano ya amani yaliyosainiwa kati ya serikali na upinzani mwezi Septemba mwaka huu.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Sudan Kusini, Michael Chiangjiek alisema baada ya kusainiwa karatasi iliyothitibisha kuachiwa huru watu hao wawili kuwa: "Tupo hapa kutekeleza maagizo ya Rais. Kuachiwa huru kwa watu hawa ni sehemu ya makubaliano ya amani na sasa wako huru."
Itakumbukwa kuwa William Endeley aliyekuwa mshauri wa Riek Machar mwezi Februari mwaka huu alishtakiwa kwa kosa la kutaka kuipindua serikali na Gatdet alihukumiwa kifo mwezi huo huo kwa makosa ya uhaini na kufanya uchochezi dhidi ya serikali.