Watu 15 wameuawa katika mapigano ya kikabila nchini Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49244-watu_15_wameuawa_katika_mapigano_ya_kikabila_nchini_sudan_kusini
Watu 15 wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika mapigano ya kikabila yaliyodumu kwa siku tatu mfululizo mkoani Jonglei, Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 03, 2018 10:57 UTC
  • Watu 15 wameuawa katika mapigano ya kikabila nchini Sudan Kusini

Watu 15 wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika mapigano ya kikabila yaliyodumu kwa siku tatu mfululizo mkoani Jonglei, Sudan Kusini.

Kaimu Gavana wa mkoa huo, Agot Alier amethibitisha kuwa, Jumanne wiki hii, kundi la wanaume wa kabila la Murle lilifanya mashambulizi katika kaunti za Duk Payuel na Bor Kaskazini. Amesema Oktoba 30, kundi la wezi wa mifugo wanaoaminika kutoka mkoa wa Boma walishambulia zizi la mifugo katika kaunti ya Poktap na Duk Payuel na kuua watu watano na kujeruhi wengine 14. Amesema wamiliki wa mifugo na vijana katika eneo hilo walifanikiwa kuwafukuza washambuliaji hao na kuokoa baadhi ya mifugo.

Kaimu Gavana huyo pia amesema, Jumatano wiki hii, kulikuwa tena na mashambulizi katika kaunti ya Bor Kaskazini ambapo watu 10 waliuawa na wengine 6 kujeruhiwa.

Riek Machar na Salva Kiir

Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.  

Hivi karibuni pande hasimu zilifikia mapatano ya amani na inatarajiwa kuwa utulivu utarejea nchini humo.