Tshisekedi na Kamerhe wajiondoa kwenye muungano wa upinzani Kongo
Baada ya kushinikizwa na wafuasi wao, viongozi wawili wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamesalimu amri na kujiondoa kwenye muungano mpya wa upinzani uliotangaza mgombea mmoja mwishoni mwa wiki.
Felix Tshisekedi, kinara wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) ambaye alikuwa mmoja wa viongozi saba waliotia saini kuundwa muungano mpya wa upinzani unaofahamika kama Lumuka ametangaza kujiondoa kwenye muungano huo, baada ya kupewa saa 48 na Katibu Mkuu wa chama hicho, Jean-Marc Kabundu kujiondoa.
Vital Kamerhe, kiongozi wa chama cha UNC ambaye amewahi kuwa Spika wa Bunge la Kongo amesema amelazimika kujiondoa baada ya kushinikizwa kufanya hivyo na wanachama wake waliofanya maandamano nje ya makao makuu ya chama hicho wakimtaka ajiondoe kwenye muungano wa Lumuka.
Siku ya Jumapili, vyama saba vya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo viliafikiana na kumteua Martin Fayulu kuwa mgombea pekee wa upinzani katika uchaguzi ujao wa urais uliopangwa kufanyika nchini humo tarehe 23 ya mwezi ujao wa Disemba.
Tayari chama tawala cha Rais Joseph Kabila kimempendekeza Emmanuel Ramazani Shadary aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo kuwa mgombea wake katika uchaguzi huo.