Wanafunzi Waislamu Nigeria waruhusiwa kuvaa Hijabu shuleni Lagos
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49530-wanafunzi_waislamu_nigeria_waruhusiwa_kuvaa_hijabu_shuleni_lagos
Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu Nigeria NSCIA limepongeza agizo la Mahakama ya Juu nchini humo la kuitaka serikali ya jimbo la Lagos kuwaruhusu wanafunzi Waislamu kuvaa Hijabu katika shule za umma katika mji mkuu huo wa kibiashara.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Nov 15, 2018 11:56 UTC
  • Wanafunzi Waislamu Nigeria waruhusiwa kuvaa Hijabu shuleni Lagos

Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu Nigeria NSCIA limepongeza agizo la Mahakama ya Juu nchini humo la kuitaka serikali ya jimbo la Lagos kuwaruhusu wanafunzi Waislamu kuvaa Hijabu katika shule za umma katika mji mkuu huo wa kibiashara.

Mahakama hiyo imesema kuwa, kesi kuhusiana na kadhia hiyo ingali inaendelea, na kwamba wanafunzi hao wa kike katika shule za umma jimboni Lagos waendelee kuvaa vazi hilo la stara, hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Baada ya Mahakama ya Rufaa katika jimbo la Lagos kutoa hukumu ya kubatilisha amri ya serikali ya jimbo hilo ya kupiga marufuku vazi la Hijabu kuvaliwa na wasichana Waislamu shuleni mnamo Februari mwaka 2016, serikali hiyo ya kieneo iliwasilisha faili la kesi hiyo katika Mahakama ya Juu.

Chama cha Wanafunzi Waislamu Nigeria MSSN pia kimepongeza uamuzi huo wa muda wa Mahakama ya Juu, na kuutaja kama ushindi mkubwa kwa mapambano ya muda mrefu ya kupigania haki ya kuabudu.

Wanawake Waislamu wa Nigeria waliovaa mavazi ya stara wakiwa katika maandamano mjini lagos

Mwaka jana, wanafunzi Waislamu katika shule moja jimboni Gun kusini magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi walieleza kusikitishwa kwao na hatua ya shule yao kuwazuia kuvaa Hijabu.

Waislamu nchini Nigeria wamekuwa wakilalamikia sheria za baadhi ya majimbo ya nchi hiyo za kupiga marufuku vazi la hijabu katika shule binafsi na za umma hasa katika maeneo ambayo wakazi wake wengi ni Wakristo.

Wanasisitiza kuwa kuvaa vazi la staha la Hijabu ni haki yao ya kikatiba ambayo inapaswa kulindwa na serikali kupitia sheria.