UN: Mapatano ya amani ya Sudan Kusini ni legelege
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya amani ametahadharisha kuwa, makubaliano ya amani ya Sudan Kusini ni tete na legelege na ni sawa na kuhifadhi fedha taslimu.
Jean-Pierre Lacroix amesema hayo na kuongeza kuwa, maadamu pande hasimu za Sudan Kusini bado zinashikilia silaha mikononi mwao na hadi hivi sasa hazijakubali kusimamisha vita kikamilifu, tusitarajie kuona mapatano hayo ya amani yanakuwa imara.
Lacroix alikabidhi ripoti yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, muda mfupi baada ya kutiwa saini makubaliano ya kutatua mgogoro wa Sudan Kusini pamoja na ziara zilizofanywa na maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini tarehe 9 Oktoba.
Kwa mujibu wa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwezi Septemba mwaka huu kati ya serikali ya Sudan Kusini na makundi ya waasi, Riek Machar, kiongozi wa wapinzani wenye silaha amerejeshewa nafasi yake ya Makamu wa Rais wa nchi hiyo.
Mapigano ya ndani nchini Sudan Kusini yalianza tarehe 15 Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumfuta kazi makamu wake wakati huo Riek Machar kwa madai kuwa amepanga njama za kumpindua. Hadi hivi sasa watu laki tatu na 85 elfu wameshauawa na mamilioni ya wengine wamejeruhiwa na kuwa wakimbizi.
Sudan Kusini ilijitenga na ndugu zao wa Sudan mwaka 2011 na tangu wakati huo hadi hivi sasa haijawahi kuwa na utulivu wa kuendelea, bali imekuwa ikisumbuliwa na mizozo hii na ile.